Skip to main content
WISN na POA Kuimarisha Huduma za Afya Katavi Na: Frank Mvungi - MAELEZO, Mbeya Mkoa wa Katavi umetajwa kunufaika na mfumo wa kubaini taarifa za mahitaji ya watumishi kwa kuzingatia uzito wa kazi, ambapo Halmashauri zote 185 na Mikoa yote Tanzania bara inanufaika na mifumo hiyo inayolenga kuimarisha huduma za afya. Akizungumza leo Jijini Mbeya wakati akifungua mafunzo kwa makatibu wa afya, maafisa utumishi, wataalamu wa takwimu za afya, na waganga wakuu wa Wilaya wa mkoa wa Katavi, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Utawala na Rasilimali Watu wa mkoa huo, Bi. Crescencia Joseph, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuzijengea uwezo Halmashauri na Mikoa ili ziweze kutumia mifumo ya WISN na POA iliyorahisishwa kuwapangia vituo vya kazi, na katika kuomba watumishi wapya kulingana na mahitaji. WISN ni mfumo unaotumika kubaini mahitaji ya watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya na vipaumbele katika maeneo husika, Wakati POA hutumika kupanga mgawanyo wa watumishi hao kulingana na uhitaji wa kila kituo, Mifumo hii miwili iko chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), pamoja na Ofisi ya Rais – Utumishi, kwa kushirikiana na Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID). Mradi huu wa miaka mitano unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania bara. “Serikali kupitia OR-TAMISEMI inatarajia kuajiri watumishi wapya 6180 wa sekta ya Afya na 1500 kutoka Wizara ya Afya, hivyo ni matarajio yangu kuwa halmashauri zitatumia ripoti za mfumo wa WISN na POA iliyorahisihwa katika kugawanya watumishi wapya kwa kuzingatia taarifa za mifumo hiyo,” alisisitiza Bi. Crescencia. Akifafanua, amesema kuwa mifumo hiyo ni ukombozi mkubwa katika kutoa huduma za afya katika maeneo yote hasa yale yaliyo pembezoni, kwakuwa itasaidia kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wananchi. Aidha, Bi. Crescencia aliwaasa washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia yale watakayojifunza ili waweze kwenda kuwatumikia wananchi katika kutoa huduma bora na zenye tija kama ilivyo dhamira ya Serikali. Pia aliipongeza OR-TAMISEMI Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mradi wa PS3 kwa kutoa mafunzo ya mfumo wa WISN na POA kwa mikoa ya Mwanza, Mara, Iringa, Tanga, Mbeya, Kigoma, Morogoro, Pwani na Mtwara. Mifumo ya WISN na POA iko chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Rais Utumishi, ikiwa ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuboresha huduma za afya hapa nchini.
Comments
Post a Comment