Kifo cha Mwalimu Mponda wa TaSUBa cha igusa Serikali Na Anitha Jonas – WHUSM 22/03/2018 Dar es Salaam. Serikali imetoa pole kwa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo kwa kumpoteza Mwalimu mahiri John Mponda aliyekuwa balozi wa tasnia ya Sanaa nchini. Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza katika ibada ya kumuaga marehemu huyo iliyofanyika katika Chuo cha TaSUBa Wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kumuaga kwani anatarajiwa kuzikwa kijiji cha Mbalizi Mkoani Mbeya. “Tunatambua mchango wa Mwalimu John Mponda katika tansia ya sanaa nchini na kupitia wanafunzi waliyopita katika mikono yake pamoja na vikundi vya vijana alivyovianzisha ambavyo amekuwa akivifundisha kazi za sanaa, hakika tumempoteza mtu makini,”alisema Mhe.Shonza. Akiendelea kuzungumza katika msiba huo Mheshimiwa Shonza aliwasihi wasanii waliyopata mafunzo kutoka kwa mwalimu huyo kuwa mabalozi kwa wasanii wenzao na kuwashauri misingi iliyobora katika katika kukuza na kuendeleza kazi za sanaa. Kwa upande wa Mkuu wa Chuo cha TaSUBa Dkt.Herbert Makoye alisema kuwa marehemu mwalimu Mponda ameondoka katika kipindi walichokuwa wanamuhitaji sana kwani kwasasa taasisi hiyo ipo katika maandalizi ya Tamasha la Utamaduni la Bagamoyo ambalo nilakimataifa na hufanyika kila mwaka na yeye alikuwa mratibu na mpaka mauti yanamfika alikuwa akiwa shughulikia maandalizi hayo. “Kwa hakika msiba huu ni pigo kwa taasisi yetu na mwalimu huyu alikuwa kiungo miongoni mwetu na alifanya kazi yake kwa weledi na kujituma alikuwa ni mtu aliyeipenda kazi yake ,’’alisema Dkt.Makoye. Pamoja na hayo nae Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi waliyosoma TaSUBa Deosonga Njelekela alisema kuwa mwalimu huyo kwao hakuwa tu kama mwalimu bali alikuwa baba na mlezi kwani na alikuwa mstari wa mbele kutoa nasaha zake kwa lengo la kutaka wanafunzi wake waweze kufanikiwa zaidi. Hata hivyo nae mtoto wa Marehemu Bi. Mery Mponda aliwashukuru watu wote waliyojitokeza kuungana nao katika msiba huo kwa imekuwa ni faraja kubwa kuona watu wakiomboleza pamoja nao baada ya kumpoteza baba yao mzazi ambaye alikuwa mlezi na nguzo ya familia.


Comments