Taarifa ya Tafiti mbalimbali zilizofanywa na Wizara ya Habari kuhusu Urithi wa Ukombozi kuwasilishwa kwa mawaziri wa Utamaduni wa nchi za Kusini mwa Afrika Na: Genofeva Matemu - WHUSM Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameahidi kufikisha taarifa ya hatua ambayo Tanzania imefikia katika harakati za kutafiti na kuhifadhi kumbukumbu za ukombozi wa Bara la Afrika kwa mawaziri wa utamaduni wa nchi za kusini mwa Afrika ili nchi hizo wanachama ziweze kuendelea na hatua nyingine ya kuchangia katika ujenzi wa kituo cha kuhifadhi kumbukumbu hizo. Waziri Mwakyembe ameyasema hayo leo Mkoani Mbeya alipofanya ziara kukagua maeneo yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na kusema kuwa serikali ipo katika mpango ambao maeneo yaliyotumika katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika yatakarabati na kurejesha muonekano wake wa awali ili yasipotezi historia. “Majengo yaliyotumika katika harakati za urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika ni sehemu ya historia na maeneo muhimu sana ambayo yanatakiwa kuboreshwa ili yaweze kuendelea kuwepo katika muonekano ule ule wa awali kwa lengo la kutokupoteza historia yake” amesema Mhe. Mwakyembe Aidha Mhe. Mwakyembe amesema kuwa serikali imechukua wajibu wake wa kubaini maeneo yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na kuwaomba viongozi wote nchi nzima kuendelea kubaini maeneo na vitu vilivyotumika katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika vilivyopo katika maeneo yao ili wizara iyaendeleze kwa maslahi ya taifa na Afrika kwa ujumla Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Paul Ntinika ameitaka programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kuzingatia na kuchukua taarifa ya vitu mbalimbali kama vile vyakula vilivyotumika, vifaa na nyimbo zilizotumika kuhamasisha ukombozi wa Bara la Afrika ili jamii ya sasa ifahamu kumbukumbu za ukombozi wa Bara la Afrika kwa undani zaidi. Naye Mratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika Bibi. Ingiahedi Mduma amesema kuwa hadi sasa programu inakusanya vitu vyote vilivyotumika wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika ambapo nyimbo 42 zilizokuwa zikihamasisha mambo ya ukombozi zimekusanywa, hotuba 78 zilizotumika wakati wa harakati za ukombozi zimepatikana, maeneo 161 yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi yameainishwa na watu 201 wamehojiwa ambao kwa namna moja ama nyingine wamepitia harakati hizo. Baadhi ya maeneo yaliyobainika Mkoani Mbeya kutumiwa na wanaharakati na wapigania uhuru wa Bara la Afrika ni pamoja na eneo la Game, Nyumba ya Binti Matola, Nyumba ya Juma Mtoto, Uwanja wa Mikutano, Sekondari ya Samora Michel, Nyumba iliyopo Iyela iliyotumiwa na Samora Michel pamoja na Nyumba za kwa Mapunda.










Comments