Viongozi Mkoa wa Iringa hamasisheni wananchi kutunza historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika – Mwakyembe Tarehe: 18/03/2018 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezi Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka viongozi wa Mkoa wa Iringa kuhamasisha wananchi wa Iringa kutunza utalii na historia ya ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuthamini nafasi iliyopewa nchi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika. Waziri Mwakyembe ameyasema hayo jana Mkoani Iringa alipofanya ziara katika mkoa huo kukagua maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa kusini mwa Afrika na kusema kuwa kihistoria Tanzania imepewa heshima kubwa na Umoja wa Afrika kutokana na mchango mkubwa iliyotoa wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika. “Zoezi la kuhifadhi nyaraka za kumbukumbu ya ukombozi wa bara la Afrika ni letu sote, linatusaidia waafrika kuandika upya historia yetu kutokana na kasi ya maendeleo ya kiteknolojia hivyo wajibu wetu sote kuwaandaa vijana ili wawe na uwezo wakuwezesha na kurithisha historia ya urithi wa ukombozi kwa vizazi vijavyo ndani na nje ya nchi” amesema Mhe. Mwakyembe Aidha Mhe. Mwakyembe amesema kuwa Mnara wa Lugalo walipozikwa askari wa kijerumani 300 na kiongozi wao ni moja ya ishara ya ushujaa na uzalendo ulioonyesha uimara wa watanzania kipindi cha harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na kuahidi kuwa serikali itayalinda, kuyatunza na kuyaendeleza maeneo yote yaliyotumika katika harakati hizo ili vizazii vya Afrika vipate fursa ya kujua historia tuliyopitia wakati wa kujikomboa. Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Amina Masenza ametoa wito kwa watanzania wote walio na habari za kihistoria kujitokeza na kuweza kutoa historia hiyo ili waweze kutenda na kutimiza wajibu woa kwa manufaa ya watanzania wote na kuijenga na kuisimamisha Tanzania kihistoria kwani historia ni jambo hai lisilokufa. Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Mhe. Asia Abdala amesema kuwa wilaya yake chini ya serikali ya awamu ya tano itahakikisha kuwa inarejesha misingi ya utamaduni wa mtanzania na historia nzuri iliyojengwa katika Bara la Afrika kwani Iringa inasifika kwa historia hiyo na kama kwa pamoja serikali kwa kushirikiana na wanairinga watayaendeleza maeneo yaliyotumika katika harakati za ukombozi utalii na uchumi wa mkoa wa Iringa vitakua. Picha na Genofeva Matemu – WHUSM










Comments