Watendaji wanaosimamia Sekta ya sanaa na Taasisi kutaneni na wasanii kuelimisha taratibu na sheria zilizopo katika sekta ya sanaa - Mwakyembe Na: Genofeva Matemu - WHUSM Watendaji wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo katika sekta ya Sanaa pamoja na Taasisi zake ikiwemo BASATA, Bodi ya Filamu na TCRA wametakiwa kukutana na makundi ya wasanii wa mziki nchini kwa lengo la kuelimisha taratibu za kuwasiliana na mamlaka husika za sanaa ili zijiridhishe na maudhui ya kazi za sanaa kabla ya kuzisambaza. Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe baada ya kufanya kikao na msani wa muziki wa bongo fleva Nassibu Abdul (Diamond) kujadili namna ya kuboresha maadili katika kazi za sanaa na baadaye kukutana na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam. Mhe. Mwakyembe amesema kuwa maamuzi ya kuzifungia baadhi ya nyimbo yamefanywa kwa mujibu wa sheria na si kwa utashi binafsi wa kiongozi wa wizara, hivyo wasanii na jamii kwa pamoja waelewe kwamba hatua zilizochukuliwa na Naibu Waziri Shonza hivi karibuni zilikuwa za Wizara kwa mujibu wa sheria za nchi. “Serikali haina ugomvi wowote na wanasanaa nchini bali ina tatizo na mmomonyoko wa maadili ya kitanzania nchini na kwamba kila mwanasanaa ana wajibu wa kulinda maadili ambayo ni sehemu ya utamaduni wetu” amesema Mhe. Mwakyembe Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza amewasisitizia wanasanaa kufuata taratibu za kuwasilisha kazi zao za sanaa mapema kwenye mamlaka husika ili kuepusha matatizo baadaye kwani suala la kulinda maadili ni endelevu. “Wakati umefika sasa kwa Bodi ya Filamu Tanzania na TCRA kukamilisha zoezi la kuoanisha kanuni za madaraja ya kazi za sanaa ili kazi zinazofaa kuonekana na watu wazima peke yake zianze kuangaliwa saa sita usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi” amesema Mhe. Shonza Naye msanii wa muziki wa Bongo Fleva Nassibu Abdul (Diamond) ameahidi kushirikiana kwa karibu na Naibu Waziri Shonza na uongozi mzima wa Wizara ya Habari katika kusimamia maadili ya kazi za sanaa na kuwa mfano bora wa wasanii nchini katika kulinda utamaduni wa mtanzania.





Comments